Shirika la Habari la Hawza | Imam wa mwisho wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na Khalifa wa Kumi na Mbili wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alizaliwa alfajiri ya Ijumaa, katika usiku wa nusu ya Shaaban mwaka 255 Hijiria (868 Miladia) katika mji wa Samarra, moja ya miji ya Iraq.
Baba yake mtukufu alikuwa ni kiongozi wa kumi na moja wa Shia, yaani Imam Hasan al-Askari (a.s), na mama yake mtukufu alikuwa ni bibi mwenye sifa njema aitwaye Nargis ambaye kuhusu utaifa wake riwaya zimekuja kwa namna tofauti. Kwa mujibu wa riwaya moja, bibi huyo alikuwa binti wa "Yashu'a" mwana wa Mfalme wa Roma, na mama yake alikuwa wa kizazi cha "Sham'oon" wasii wa Nabii Isa (a.s). Kulingana na riwaya hii, Nargis, baada ya kuona ndoto ya ajabu, alisilimu, na kwa uongofu wa Imam Hasan al-Askari (a.s), alijiweka kati ya jeshi la Warumi waliokuwa wakielekea kupigana vita dhidi ya Waislamu, na pamoja na kundi jingine akachukuliwa mateka na jeshi la Kiislamu. Imam Hadi (a.s) alimtuma mtu akamnunua na kumleta Samarra.
Pia riwaya nyinginezo zimepokelewa, lakini jambo la muhimu na la kuzingatia ni kwamba Bibi Nargis (s.a) alikaa kwa muda katika nyumba ya Bibi Hakima Khatun (s.a) — mmoja wa dada wa heshima wa Imam Hadi (a.s) na alilelewa na kufundishwa chini ya uangalizi wake, akiwa na heshima kubwa mbele yake.
Bibi Nargis (s.a) ndiye bibi ambaye miaka mingi kabla, katika maneno ya Mtume wa Uislamu (s.a.w.w), Amir al-Mu’minin (a.s), na Imam Ja'far al-Sadiq (a.s), alisifiwa na kutajwa kama mbora wa vijakazi na bibi wa vijakazi wote.
Inapaswa kusemwa pia kwamba, mama wa Imam wa zama (a.f) alikuwa akijulikana kwa majina mengine kama: Sawsan, Rayhana, Malika, na Sayqal (Saqil).
Jina, Kuniya na Lakabu
Jina na kunia (kuniya) ya Imam wa Zama (a.s) ni sawa kabisa na jina na kunia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), na katika baadhi ya riwaya imekatazwa kulitaja jina lake hadi wakati wa kudhihiri kwake.
Lakabu mashuhuri za Imam huyo ni: Mahdi, Qa’im, Muntadhir, Baqiyyatullah, Hujjat, Khalaf Swalih, Mansur, Sahibu al-Amr, Sahibu al-Zaman, na Waliyy al-Asr, ambapo mashuhuri zaidi kati ya zote ni Mahdi.
Kila moja ya lakabu hizi ina ujumbe maalumu kumhusu mkubwa huyu.
Imam huyu wa kheri huitwa Mahdi, kwa sababu yeye ni aliyepata uongofu na huwaongoza watu kuelekea haki; na huitwa Qa’im, kwa sababu atainuka kwa ajili ya haki; na huitwa Muntadhir, kwa sababu watu wote wanangoja kuja kwake; na huitwa Baqiyyatullah, kwa sababu yeye ni mabaki ya hoja ya Mola na hazina ya mwisho ya Mwenyezi Mungu.
Hujjat maana yake ni hoja ya Mwenyezi Mungu juu ya viumbe Wake, na Khalaf Swalih, maana yake ni mrithi mwema wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mansur, kwa sababu hupata msaada kutoka kwa Mola wake. Yeye ni Sahibu al-Amr, kwa sababu jukumu la kuasisi serikali ya haki ya Mwenyezi Mungu liko mikononi mwake. Sahibu al-Zaman na Waliyy al-Asr humaanisha kuwa yeye ndiye mtawala na kiongozi wa enzi hiyo.
Maisha ya Imam Mahdi (a.s) yanajumuisha vipindi vitatu vyenye mabadiliko makubwa:
1. Kipindi cha Kujificha: Maisha ya faragha ya Imam kuanzia kuzaliwa kwake hadi kufa kwa Imam Hasan al-Askari (a.s).
2. Kipindi cha Ghaiba: Kuanzia wakati wa kufa kwa Imam wa Kumi na Moja (a.s) na kitaendelea hadi atakapodhihiri kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
3. Zama za Kudhihiri: Baada ya kipindi cha ghaiba kupita, kwa mapenzi ya Mola wa ulimwengu, Imam wa Kumi na Mbili (a.s) atadhihiri na kuja kuijaza dunia wema na uzuri. Hakuna anayejua wakati wa kudhihiri kwa Imam huyo Aliyeahidiwa, na imepokewa kutoka kwa Imam wa Zama (a.s) kuwa; wale wanaotaja wakati wa kudhihiri kwake ni waongo.
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka kwenye kitabu kiitwacho "Nengini afarinesh" huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Maoni yako